Tuesday, August 21, 2012

FUATA KANUNI HII, ILI USIUGUE.





TUMESHAANDIKA mambo mengi kuhusu umuhimu wa mtu kula matunda, mboga na vyakula vya nafaka, leo tunaandika muhtasari wa kanuni za ulaji sahihi ambazo zikizingatiwa na zikaenda sambamba na ulaji wa vyakula vinavyokubalika kiafya, kutakuwa hakuna shaka kuhusu ujenzi wa msingi imara wa afya bora na huenda usiugue mara kwa mara.
USILE CHAKULA KINGI KUPITA KIASI
Kila mtu anakula chakula kulingana na mahitaji ya mwili wake. Mbeba zege hawezi kula sawa na anayefanyakazi ya kukaa ofisini, kula kiasi ambacho kinalingana na mahitaji ya mwili wako. Kanuni ya kula inasema acha kula wakati bado hujashiba vizuri. Kwa kawaida mahitaji ya chakula ya mwili ni kiasi cha ‘kalori’ 2000 kwa siku, ikitegemeana na umri, jinsi, urefu, uzito na kazi anazozifanya mtu.
KULA VYAKULA MCHANGANYIKO
Ulaji sahihi ni ule wa kula vyakula mchanganyiko vya aina tofauti, hasa mboga za majani, matunda, vyakula vya nafaka ambavyo huwa huvili mara kwa mara. Kwa kula vyakula mchanganyiko utapata faida ya kuwa na virutubisho tofauti mwilini na kuondoa upungufu wowote wa vitamini unaoweza kuwepo mwilini bila wewe kujijua.

KULA SANA MATUNDA NA MBOGA
Ni kawaida ya watu wengi kutokula matunda kabisa katika staili yao ya maisha ya kila siku, ikitokea amekula tunda au mboga ni kwa bahati mbaya tu. Hili ni kosa kubwa sana unaloweza kuwa unalifanya katika afya yako ambalo baadaye lina kukagharimu sana bila kujua chanzo chake ni kutokula matunda.
Hivyo hakikisha siku haipiti bila kula matunda na mboga. Kiwango kinachopendekezwa na Shirika la Afya Duniani, ni kwa mtu mmoja kula mara kwa mara matunda na mbogamboga kati ya mara 4 na 6 kwa siku, mlo mmoja unaweza kuwa sawa na ujazo wa kisahani cha chai.


 KUNYWA MAJI MENGI
Kama kuna kosa lingine kubwa unaloweza kulifanya katika mwili wako ni kutokunywa maji. Haishangazi kuona mtu hana mazoea ya kunywa maji hadi pale anapopatwa na kiu na akinywa ni glasi moja tu.
Imeelezwa na wataalamu wetu kuwa asilimia 75 ya mwili wa binadamu ni maji. Unywaji wa maji ya kutosha kila siku nayo ni sehemu ya ulaji sahihi. Maji ndiyo yanayosaidia kusafisha mifumo ya mwili na kutoa nje uchafu na sumu, hasa kwenye kibofu cha mkojo na figo. Watu wanaopatwa na matatizo ya viungo hivyo ni wale wenye tabia ya kutokunywa maji ya kutosha kwa muda mrefu.

PUNGUZA KULA VYAKULA VYENYE SUKARI
Ili kuwa na afya bora, epuka ulaji wa vyakula vyenye sukari au punguza kiwango cha sukari unachoweka kwenye vinywaji ama vyakula vyako unavyopika. Inaelezwa kuwa unywaji wa soda moja tu kwa siku, huweza kuongeza uzito wa mwili kwa kilo 10 kwa mwaka, kwa sababu soda ni miongoni mwa vinywaji vyenye sukari nyingi.

KUWA HURU NA VYAKULA
Iwapo utazingatia ulaji sahihi, bila shaka utakuwa huru kula mara moja moja vyakula vingi, hata vya kukaanga bila kupata matatizo yoyote. Kwani chakula ni chanzo kizuri cha furaha na mtu mwenye furaha hujiepusha na magonjwa ya moyo pia.

JISHUGHULISHE
Mwisho, ili lishe yako au ulaji wako sahihi ufanyekazi yake vizuri na kukupa afya njema, lazima ufanye mazoezi au ujishughulishe na kazi mbalimbali za kila siku. Kula vizuri bila kuushughulisha mwili, hakuwezi kuwa na faida kiafya. Aidha, katika hili mambo matatu hayana budi yazingatiwe, nayo ni Lishe Bora, Mazoezi na Kupumzika.

No comments:

Post a Comment