Monday, March 18, 2013

Ni Ambassadors Christ kwenye Tamasha la Pasaka,utakuwa wapi?



KUNDI la muziki wa kiroho la Ambassadors of Christ ‘Kwetu Pazuri’ la Kigali, Rwanda linatarajia kuzindua albamu mpya iitwayo Kaeni Macho, Machi 31, mwaka kwenye Tamasha la Pasaka.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama alisema Dar es Salaam jana kuwa kundi hilo limemhakikishia kwamba albamu hiyo itakuwa moto wa kuotea mbali.
Alizitaja nyimbo zilizopo kuwa ni Kaeni Macho, Mungu Wangu, Tugireurukundo, Ewe Ndugu, Tuombeane, Umwamini Yesu, Msalaba, Twawona, Okuswala na Huruma.
“Kundi hilo maarufu kwa jina la Kwetu Pazuri, limefurahi sana kuja hapa Tanzania na wamenieleza albamu hiyo hawajawahi kuizindua hivyo ni baraka kubwa kwa Watanzania kupewa heshima hiyo,” alisema Msama na kuongeza kuwa kundi hilo pia litatumbuiza katika maonyesho mengine ya mikoani.
Kwa mujibu wa Msama hivi sasa kundi hilo linatamba na albamu ya Mtegemee Yesu na wamemhakikishia kuwa watang’arisha tamasha la mwaka huu na wamejipanga vya kutosha kuhakikisha mashabiki wanapata burudani ya nguvu.
Alisema albamu yao hiyo ina nyimbo nane ambazo ni JY’ Ushima Uwite, Mtegee Yesu, Ndifuza Kugerayo, Iyana Iby’ Isi, Yesu Niwe Mungeri, Parapanda, Abasaruzi na Nenda.
Licha ya kundi hilo, wasanii wengine wa nje ya Tanzania watakaotumbuiza tamasha hilo ni Sipho Makhabane wa Afrika Kusini, Ephraim Sekeleti wa Zambia na Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya.
Wasanii wa Tanzania waliothibitisha hadi sasa ni Rose Muhando, Upendo Nkone, John Lissu, Kwaya ya Kinondoni Revival na kundi la Glorious Celebration.
Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es Salaam Machi 31, na litaendelea Aprili Mosi kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, wakati Aprili 3 ni Uwanja wa Samora, Iringa, Aprili 6 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

No comments:

Post a Comment